Kocha Msiaidizi wa Mbeya City FC Noliega Mwamlima amesema kikosi chao kipo tayari kuikabili Simba SC kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mbeya City itakua Mgeni wa Simba SC kwenye mchezo huo utakaopigwa Jumanne (Januari 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam majira ya saa moja usiku.
Kocha Mwamlima amesema maandalii yao kuelekea mchezo huo yana ari kubwa, na wachezaji kila siku wamekua wanaonesha wanazihitaji alama tatu dhidi ya Simba SC, japo amekiri haitakuwa rahisi.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo wetu dhidi ya Simba SC, tupo Dar es salaam tukiendelea na maandalizi yetu kuelekea mchezo huo ambao tunaamini utakua mzuri na wenye ushindani mkubwa.”
“Wachezaji wetu wote wamekuwa wakihizana kupambana kwenye mchezo huo, wanajua wanaweza kuimudu Simba SC kama tulivyofanya kwenye mchezo wa Duru la kwanza nyumbani Mbeya, japo vikosi vyote vitakuwa na maingizo ya wachezaji tofauti na wale waliocheza mchezo wa kwanza uliomalizika kwa sare ya 1-1.” amesema Mwamlima
Mbeya City itaingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Simba SC ikikumbuka matokeo mabaya walioyapata mbele ya Azam FC kwenye mchezo wao wa mwisho uliopigwa Uwanja wa Azam Complex-Chamazi.
Mchezo huo uliopigwa Desemba 30-2022, ulishuhudia Mbeya City ikifungwa mabao 6-1.
Upande wa Simba SC, wanakumbuka kisago walichokiacha kwa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ cha 7-1, Desemba 30-2022, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mchezo dhidi ya Mbeya City, utakua wa kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ tangu alipoanza kazi na Klabu hiyo mwishoni mwa juma lililopita.