Leo ni maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kwa mwaka huu hakutakuwa na gwaride kama ilivyozoeleka na fedha zilizotengwa kwa shughuli hiyo, zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya sekta ya elimu Zanzibar.

Mapinduzi hayo, yalitokea mwaka 1964 ili kumuondoa madarakani Sultani wa Zanzibar na serikali yake, iliyoundwa hasa na Waarabu, na hatimaye kuweka uongozi mikononi mwa Waafrika, ambao ndio wengi visiwani humo (230,000 hivi), kwenye bahari ya Hindi, karibu na pwani ya Tanganyika.

Usultani wa Zanzibar ulikuwa umepewa na Uingereza uhuru wake mwaka 1963 lakini kabla ya hapo, Waarabu walikuwa wamefaulu kudumisha katika mfululizo wa chaguzi utawala waliokuwa nao tangu zamani za Zanzibar kuwa chini ya Usultani wa Omani.

Mwanamapinduzi na Mwanachama wa ASP, John Okello. Picha ya JMT.

Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilichowakilisha hasa Waafrika, kilipoona kwamba bungeni kina viti vichache ingawa kilipata 54% za kura katika uchaguzi wa Julai 1963, kilipatana na chama cha mrengo wa kushoto Umma Party.

Januari 12, 1964 Mwanachama wa ASP John Okello (1937-1971), kutoka Uganda aliongoza wanamapinduzi 600–800 wa kisiwa kikuu cha Unguja kushinda polisi wa nchi na kuteka silaha zao kisha walielekea Zanzibar na kumpindua Sultani Jamshid bin Abdullah na serikali yake.

Waliokufa katika mapigano hayo wanakadiriwa kufikia watu 80 na Kiongozi wa ASP Abeid Karume, asiyekuwa na msimamo mkali akawa rais wa kwanza wa Zanzibar huku wanachama wengi wakipewa nafasi serikalini.

Abeid Karume (kulia), na Mwl. Julius Nyerere (kushoto), Picha ya JMT.

Kufikia mwezi Machi, Okello alikuwa ameshawekwa pembeni na baadaye mwezi Aprili kikosi chake kilikuwa tayari kimeshanyang’anywa silaha na mwelekeo wa Kikomunisti wa baadhi katika serikali mpya uliogopesha nchi za Magharibi.

Kwa kuwa Zanzibar ilikuwa chini ya athari ya Uingereza, serikali yake iliandaa mipango kadhaa lakini hata hivyo, hofu ya kuundwa kwa serikali ya Kikomunisti haikutimia kamwe, na kwa kuwa wananchi wa Uingereza na Marekani waliweza kuhama bila shida, mipango hiyo haikutekelezwa.

Hata hivyo, Wakati huo nchi za Kikomunisti za China, Ujerumani Mashariki na Umoja wa Kisovyeti zilianzisha mahusiano ya kirafiki na serikali mpya ya Zanzibar kwa kuitambua rasmi na kwa kutuma washauri.

Jamshid bin Abdullah al-Said utawala wake ulifikia tamati Januari 1964 alipopinduliwa katika mapinduzi ya Zanzibar. Picha ya CPA Media/Alamy

Karume alifanikisha majadiliano ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika na hatimaye muungano wa Tanzania ulifanikiwa huku vyombo vya habari vikitafsiri muungano huo kuwa juhudi za kuzuia Ukomunisti kuibadilisha Zanzibar.

Mapinduzi hayo, yalikomesha miaka 200 ya utawala wa Waarabu Zanzibar, na yanaadhimishwa kila mwaka kama sikukuu ya taifa zima la Tanzania.

Tanzania Prisons yatuma salamu Azam Complex
Kocha Mbeya City: Tunaimudu Simba SC