Aliyekua Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amejibu taarifa zilizosambaa kwa kasi jana Alhamis (Januari 05), zikidai hayuko tayari kufanya kazi na Kocha Robertinho.
Mgunda alikaimu nafasi ya Kocha Mkuu tangu Septemba 2022, baada ya kuondoka kwa Kocha Zoran Maki aliyetimkia Misri.
Mgunda amejibu taarifa hizo baada ya kurejea jijini Dar es salaam leo Ijumaa (Septemba 06), akitokea Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’, ambako kikosi chake kilishiriki Michuano ya Kombe la Mapunduzi 2023.
Kocha huyo mzawa wamesema suala la kuletwa Kocha Mkuu ni la kawaida katika Soka, huku akiahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na Robertinho, aliyekabidhiwa jukumu la kuivusha Simba SC hadi kwenye mafanikio msimu huu 2022/23.
“Ni jambo la kawaida kwenye mpira, nitafanya naye kazi kwa ushirikiano mkubwa kwa maslahi ya Simba SC.” amesema Mgunda
Mguda alianza kazi Simba SC wakati wa Mchezo wa mkondo wa Kwanza wa kuwania kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullet ya Malawi, na kuibuka na ushindi ugenini wa 2-0, kabla ya kufanya hivyo tena Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mchezo wa pili wa Michuano hiyo aliibamiza Primeiro de Agosto ya Angola kwa kuifunga ugenini mabao 3-1, na mchezo wa Mkondo wa pili uliopigwa Dar es salaam alishinda 1-0.
Katika Ligi Kuu Mgunda amepoteza mchezo mmoja dhidi ya Azam FC kwa kushuhudia kikosi chake kikifungwa 1-0, huku akitoa sare mbili dhidi ya Mbeya City na Kagera Sugar.