Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin amesema mchezo wa Pili wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Suez SC utatoa Picha halisi ya kikosi chake, baada ya kufanya maandalizi kwa zaidi ya juma moja nchini Misri.
Azam FC leo Jumanne (Agosti 02) itacheza mchezo huo wa Kirafiki, huku ikiwa na lengo la kuwaweka sawa wachezaji wake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Kocha Moallin amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Wadi Degla kwa kufungwa 1-0.
Kocha huyo kutoka nchini Marekani mwenye asili ya Somalia amesema, kwa kushirikiana na Benchi lake la Ufundi amefanya maboresho katika kikosi chake, baada ya kuona mapungufu kadhaa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Wadi Degla.
“Leo tutaona picha kamili ya maandalizi yetu hapa Misri ambayo yana muda wa zaidi ya juma moja, tunajua mchezo dhidi ya Suez SC utakua na ushindani na utawasadia wachezaji wangu kuonyesha uwezo wao,”
“Mpango mkuu ni kuwa na kikosi Bora, na sisi kama Azam FC kikosi hicho tunacho kwa ajili ya kushindana msimu ujao, tupo hapa kwa ajili ya kukiweka sawa, kupitia michezo hii ya Kirafiki itatusaidia sana kuwa na kitu cha kwenda kukitumia katika msimu mpya wa Ligi ya Tanzania.”
“Tunataka kuona Maendeleo, Tunataka kuona Mabadiliko, Tunataka kuona Mambo ambayo yataleta kitu Kipya katika harakati zetu za kupambania Ubingwa wa Ligi ya Tanzania, naamini kuna kitu kitakwenda kuonekana baadae leo Jumanne.” amesema Kocha Moallin.
Mbali na kuweka malengo ya kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, Azam FC imejipanga kufanya maajabu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’ msimu ujao 2022/23.