Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, ametangaza neema ya furaha kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, baada ya kurejea kwa Mshike Mshike wa Ligi kuu Tanzania Bara 2021/22.
Ligi Kuu ambayo itaingia mzunguuko wa tatu baadae mwezi huu Oktoba, imesimama kupisha michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, zitakazounguruma nchini Qatar.
Kocha Nabi anaamini neema ya furaha itapatikana kwa Mashabiki na Wanachama kufuatia Program alizojiwekea katika kipindi hiki, ambacho amedhamiria kukinoa kisawasawa kikosi chake kabla ya kurejea kwa michezo ya Ligi Kuu.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema: “Kitu cha kwanza ambacho kwetu ni bora ni kuwa bado tumepata matokeo mazuri katika mechi tatu, kuanzia ile ya Simba na mbili za ligi ingawa bado tumekuwa na shida katika kipindi cha pili kwa kukosa muunganiko na nguvu za kushambulia.”
“Lakini matumaini yetu hili jambo litafikia kikomo kwa kuwa tunaenda Arusha kwa ajili ya kambi maalum katika kipindi hiki kifupi cha mapumziko, tunaamini tutarejea tukiwa kwenye ubora mkubwa.
“Tunajua ligi ni ngumu na imekuwa na ushindani mkubwa, lakini tunataka kuona ukubwa na nguvu ambayo tunaanza nayo ndiyo tutamaliza nayo, hivyo mashabiki wanapaswa kutulia.
Young Africans imeanza vyema Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzichapa Kagera Sugar na Geita Gold FC bao 1-0 kila mmoja, na kujikusanyia alama 6 kabla ya kusimama kwa Ligi, kupisha michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.