Kikosi cha Young Africans huenda kikacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/22.

Ligi Kuu ambayo itaingia mzunguuko wa tatu baadae mwezi huu Oktoba, imesimama kupisha michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, zitakazounguruma nchini Qatar.

Taarifa zinaeleza kuwa Uongozi wa Young Africans, upo kwenye mzungumzo na Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana, ili kufanikisha mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakao vikutanisha vikosi vya pande hizo mbili.

Mmoja wa mabosi wa Young Africans ambaye hakutaka jina lake lianikwe hadharani, amethibitisha kuendelea kwa mazungumzo na timu mbili kutoka nje ya nchi zitakazokuja nchini kucheza michezo ya kirafiki.

Kiongozi huyo amesema kati ya timu hizo mbili mojawapo ni Asante Kotoko ambayo bado hawajathibitisha kuja nchini.

“Bado Kotoko hawajathibitisha ujio wao hapa nchini kwa ajili ya kuja kucheza mchezo wa kirafiki, licha ya kuwapa taarifa na kuonyesha nia ya kukubali kuja.

“Mazungumzo yanakwenda vizuri hivi sasa na kama wakithibitisha kwa haraka, basi tutatangaza rasmi mchezo huo wa kirafiki tutakaoucheza kama siyo Arusha basi Dar.”

“Pia uongozi upo katika mazungumzo ya mwisho na moja ya timu kubwa kutoka nje ya nchi itakayokuja nchini kucheza mchezo wa kirafiki, kwani kocha ameomba michezo miwili ya kirafiki pekee.” amesema kiongozi huyo

Akithibitisha hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli amesema kuwa: “Ni kweli kocha ameomba michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa.

“Michezo hiyo ameiomba kwa ajili ya kutumia vema muda huu ambao ligi imesimama kutengeneza fitinesi na muunganiko wa timu, kuhusu timu tutakayocheza nayo tutaiweka wazi hivi karibuni.”

Young Africans imeanza vyema Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzichapa Kagera Sugar na Geita Gold FC bao 1-0 kila mmoja, na kujikusanyia alama 6 kabla ya kusimama kwa Ligi, kupisha michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.

Kocha Nabi aahidi furaha 2021/22
Simba SC yaanika mipango ya kuisasambua Jwaneng Galaxy