Baada ya Klabu ya Namungo FC kuinasa saini ya mshambuliaji, Alidor Kayembe kutoka kwa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia Red Arrows, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Hanour Janza amesema nyota huyo ndiye atakayekuwa chaguo lake la kwanza kwenye eneo hilo.
Janza amesema licha ya kiwango kizuri kinachoonyeshwa na mshambuliaji wake, Reliants Lusajo ambaye ni kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara (3) ila anaamini anaweza kucheza kama mshambuliaji namba mbili au kutokea pembeni.
“Nimewahi kufanya hivyo hata kabla ya Kayembe hajaja, uzuri wa Lusajo anaweza kucheza maeneo mengi uwanjani na akafunga hivyo nitakapoanza kuwatumia wote tegemea hayo mabadiliko kwani malengo ni kuongeza ubunifu pale mbele,” amesema Janza.
“Kayembe amepata vibali vyake vyote vinavyomruhusu kuaza kucheza nchini lakini sitomtumia haraka kwa sababu bado ni mgeni na mimi nataka aingie kwenye mfumo taratibu.”
Janza ameongeza Kayembe ataanza kumpatia dakika kadhaa za kucheza ili kuendana na wenzake kama alivyofanya kwa nyota wengine wa kigeni beki Mghana, Emmanuel Asante aliyetokea Bechem United na kiungo mkabaji kutoka Togo, Seidou Blandja aliyetoka Mbabane Swallows.
Kayembe msimu uliopita akiwa Arrows alifunga mabao nane nyuma ya kinara wa na mfungaji wa Ligi Kuu ya Zambia, Ricky Banda aliyemaliza na 16.