Baada ya kuwa na mwanzo mzuri katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, Uongozi wa Singida Big Stars amesisitiza mwendelezo wa kufanya vizuri ili kumaliza katika nafasi za juu.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu kutoka Uholanzi Hans van der Pluijm ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Mabingwa watetezi Young Africans wanaoshika nafasi ya pili, huku Simba SC ikiwa kileleni baada ya kushinda michezo miwili.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Singida Big Stars Dismas Ten amesema wanafahamu Ligi ya msimu huu ina changamoto kubwa ya ushindani, lakini Uongozi umepanga mipango mikubwa ya kuhakikisha timu yao inamaliza katika nafasi tatu za juu.

Ten amesema Uongozi wao umekua karibu na Benchi la Ufundi ili kufahamu nini kinachohitajika kuifanya timu yao kuendelea kufanya vizuri, hivyo timu yoyote watakayokutana nayo kwenye Mshike Mshike wa Ligi hiyo inapaswa kujipanga.

“Sisi hatuangalii mchezaji mmoja bali tunafurahishwa na mwenendo wa timu kwa ujumla na hatumfungi mmoja, yeyote tutakayekutana naye ajiandae.”

“Tuna malengo yetu na tunahitaji kufanya vizuri, kwa hiyo kujua nafasi ngapi tuwaachie Benchi la Ufundi ila uongozi tumejipanga kutoa sapoti ili kufikia malengo.” amesema Dismas Ten

Singida Big Stars imecheza michezo miwili na kushinda yote ikichapa Tanzania Prisons 1-0, kisha mchezo wa pili ikailaza Mbeya City 2-1.

Afisa Mipango abaka mtoto ndani ya gari, afikishwa Mahakamani
Makamu wa Rais amfariji mjane wa Mrema