Kocha Mkuu wa Rivers United ya Nigeria Stanley Eguma ameitumia salamu Young Africans kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kusema michuano hiyo ndiyo kitu pekee cha msingi kwake.

Young Africans itaanzia ugenini Nigeria kupapatuana na Rivers United April 23 mjini Port Harcourt, Nigeria kabla ya kurejea nyumbani jijini Dar es salaam kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa April 30.

Kocha Eguma Eguma amesema malengo yake makubwa ni kuona wanacheza Fainali ya michuano hiyo msimu huu 2022/23, hivyo hawezi kuona ugumu wa kucheza na timu yoyote katika hatua waliyofika kwa sasa.

“Sina sababu ya kufikiria juu ya mchezo wetu wa robo fainali dhidi ya Yanga kwa sababu ni timu ambayo tunaifahamu, tulikutana msimu uliopita na kuwatoa, kitu kikubwa ambacho nataka kuona nafika fainali msimu huu.

“Yanga siyo timu mbaya, kama wapinzani lazima tuwape heshima, lakini sioni sababu yoyote ya wao kuharibu mipango yetu na tushindwe kufikia malengo,” amesema Eguma.

Young Africans ilitinga Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikiongoza Kundi D, huku Rivers United ikimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B.

Serikali kuja na dira ya Taifa matumizi Nishati safi ya kupikia
Mbappe akomaa na Lionel Messi PSG