Wakati taarifa zikieleza Mshambuliaji Moses Phiri huenda akaondoka Msimbazi mwishoni mwa msimu huu, Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema bado anahitaji huduma ya mshambuliaji huyo kutoka Zambia.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 10 msimu huu kwenye Ligi Kuu, amekuwa akisota benchi tangu ujio wa kocha huyo raia wa Brazil kwenye kikosi cha Simba SC, huku akidaiwa kuutaka Uongozi umuachie aondoke kwenye kikosi cha wekundu hao wa Msimbazi.
Meneja wa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa Robertinho bado anahitaji huduma ya Mshambuliaji huyo na hiyo ni kutokana na rekodi zake nzuri za mabao alizokuwa nazo msimu huu.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa anatambua timu hiyo ina mpango wa kukiboresha kikosi chao kwa kusajili washambuliaji wa nguvu lakini hiyo itakuwa ni kipimo kingine kwa Phiri kumthibitishia Robertinho kuwa ni mchezaji mwenye ubora wa kuichezea Simba SC.
Amesema hata uongozi una imani kubwa na mshambuliaji huyo.
Phiri aliyejiunga na kikosi cha Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Zanaco FC ya kwao Zambia, mkataba wake na Simba SC unamalizika mwishoni mwa msimu ujao.