Kikosi cha Coastal Union kimepania kuifunga Azam FC katika mchezo wa Mzunguuko wa 29 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kujihakikishia kuendelea kucheza Ligi Kuu msimu ujao 2023/24.

Msemaji wa timu hiyo, Jonathan Tito amesema kuwa mchezo huo wameupa uzito mkubwa sababu kama ikitokea wamefungwa kutakuwa na asilimia nyingi za kuangukia mechi za mtoano (play-off) kitu ambacho hawakitaki kiwatokee.

“Kuna vitu viwili vinatufanya tulazimike kushinda mchezo huo, kwanza ni kujihakikishia kubaki Ligi Kuu msimu ujao lakini cha pili huo utakuwa mchezo wetu wa mwisho kucheza uwanja wa nyumbani Mkwakwani kwa hiyo lazima tushinde ili tuwaage kwa furaha mashabiki zetu,” amesema Tito

Msemaji huyo amesema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri chini ya kocha wao, Fikiri Elias na matumaini ya ushindi ni makubwa licha ya kwamba wanatambua ubora wa wapinzani wao Azam FC.

Amesema wanajivunia rekodi nzuri ya kuifunga Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani hivyo pamoja na ugumu wa wapinzani wao lakini anaamini alama tatu zitabaki Tanga.

CCM inahitaji katiba bora, yenye manufaa - Chongolo
Kocha Robertinho kukomaa na Moses Phiri