Uongozi wa Simba SC utalazimika kuwahi muda wa Dirisha Dogo la Usajili ili kufanikisha agizo la Kocha Mkuu wa Klabu hiyo Robert Oliviera ‘Robertinho’, ambaye anahitaji Mshambuliaji mpya.
Kocha ‘Robertinho’ tayari ameanza majukumu ya kukinoa kikosi cha Klabu hiyo jana Jumapili (Januari 08), baada ya kikosi chake kuweka Kambi Dubai-Falme za Kiarabu.
Kocha huyo amesema ili atimize malengo yake ndani ya Simba SC anahitaji Mshambuliaji mwingine ambaye anaona ataendana na falsafa zake.
Robertinho amesema Washambuliaji waliopo kwenye Kikosi Cha Simba SC ni wazuri lakini anahitaji mwingine mwenye nguvu, Kasi na maarifa ya kufunga tofauti na waliopo hivi sasa.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kupitia SimbaAPP, Uongozi wa Klabu hiyo umethibitisha kuingia sokoni ili kukamilisha agizo la Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62.
Simba SC ndio Klabu pekee inayoendelea kuonesha ushindani wa kweli dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, kwenye mbio za Ubingwa msimu huu, ikiachwa kwa alama sita, huku ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Klabu hiyo ya Msimbazi pia ina kazi kubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi, ikipangwa Kundi C lenye timu za Vipers SC (Uganda), Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco).
Simba SC imeweka malengo ya kufika Nusu Fainali kwenye Michuano hiyo mikubwa katika ngazi ya vilabu Barani Afrika, baada ya kutinga Robo Fainali kwa zaidi ya mara moja ndani ya miaka mitano iliyopita.