Kocha Msaidizi wa Singida Big Stars Mathias Lule amesema tangu walipowasili jijini Dar es salaam kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans, kikosi chao kipo safi na salama.

Singida Big Stars itapapatuana na Young Africans kesho Jumatano (Novemba 17), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mishale ya saa moja usiku, huku ikiwa na kiu ya alama tatu ambazo zitawaongezea morari ya kuwania nafasi nne za juu kwenye Msimamo.

Lule amesema wachezaji wote wameonesha kuwa tayari kwa mchezo huo, na wamedhamiria kupambana ili kufikia lengo la kushinda na kuvunja Rekodi ya Young Africans ya UNBEATEN.

Amesema wameifuatilia Young Africans tangu ilipokabiliwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kisha Ligi kuu dhidi ya Kegara Sugar uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

“Michezo yao yote tukianza na ule wa Kimataifa hadi ule wa Kagera Sugar kuna vitu ambavyo tumeviona na kuvifanyia kazi, hata vilivyobadilika tumevifanyia kazi.”

“Walivyocheza kwenye michezo hiyo miwili huenda wasicheze hivyo kwenye mchezo wetu wa kesho, hali kadhalika hata sisi tulivyocheza dhidi ya Simba SC huenda tusicheze vile tena, kwa hiyo tunajua namna ambavyo tumejipanga ili kufanikisha mapambano yanatupa faida ya ushindi.” amesema Lule

Kwenye Michezo 10 iliyocheza Singida Big Stars imeshinda mitano, sare tatu na kufungwa miwili ikiwa nafasi ya nne ikifikisha alama 18, huku Young Africans iliyocheza michezo tisa imeshinda saba na sare mbili ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ufaransa yaanza safari ya QATAR
Watano wafungiwa leseni kwa ulevi, mwendokasi