Licha ya kuanza na ushindi katika mechi ya kwanza, Kocha Mkuu wa timu ya Kenya, ‘Harambee Stars’, Francis Kimanzi amefungiwa michezo miwili na kamati ya maandalizi ya michuano ya Baraza la Vyama vya soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Kimanzi amesimamishwa kwa tabia isiyokuwa ya kimichezo baada ya kuwahamasisha wachezaji wa timu yake kususia kucheza mchezo dhidi ya Tanzania Bara kwa madai kuwa wachezaji watatu wa timu pinzani walikuwa hawana paspoti halali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alisema Kimanzi hatakiwi hata kufika uwanjani kutazama mechi hadi atakapomaliza adhabu yake.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 11 (5) cha sheria na kanuni za mashindano haya, Kimanzi amesimamishwa michezo minne kuwa kwenye benchi la ufundi pia hatoruhusiwa kuingia uwanjani kutazama mechi yoyote hadi amalize adhabu yake,” alisema Musonye.
Musonye alisema iliripotiwa kuwa Kimanzi na benchi la ufundi la Kenya waliwashawishi wachezaji wasicheze na Tanzania na kuwafungia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa madai wachezaji watatu wa Tanzania Bara hawakuwa na paspoti halali.
Pia msaidizi wake, Zedekia Otieno amepewa onyo kwa tabia yake isiyokuwa ya kimchezo kwa kumfungia nje mwamuzi wa akiba Mohamed Guedi.
Katika mchezo huo mabingwa hao watetezi waliifunga Tanzania Bara kwa bao 1-0 lililofungwa na Hassan Abdallah dakika ya nne.