Kocha Mkuu wa USM Alger Abdelhak Benchikha amesema anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Young Africans huku akimtaja Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanapaswa kuchungwa.
Kesho Jumapili (Mei 28) USM Alger wanatarajiwa kuvaana na Young Africans katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kabla ya kurudiana tena juma lijalo nchini Algeria.
Young Africans wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Marumo Gallants katika michezo miwili ya hatua ya Nusu Fainali ya mashindano hayo.
Benchikha amesema: “Tunatarajia mchezo mgumu hasa kutokana na ubora ambao Young Africans waliuonyesha kwenye mashindano haya kupitia michezo yao iliyopita ambayo tumepata nafasi ya kuitazama.
“Wamekuwa na rekodi nzuri kwenye uwanja huu wa nyumbani na wana wachezaji bora kama namba tisa wao Mayele ambaye anaongoza kwenye ufungaji, lakini tayari tumeandaa mpango wa kuwazuia na tunaimani tutashinda.”
Katika taarifa nyingine ambazo Dar24 Media imezinasa ni kuwa Waarabu hao wamekuja kwenye mchezo huo wakiwa kamili kwa kila kitu ikiwemo kuwa na wapishi watano.
“Kwenye msafara huu, jamaa wamekuja na vyakula, mbali na vyakula pia taarifa rasmi ni kuwa kuna zaidi ya wapishi watano wamekuja na msafara huo, hii yote ni kuepuka chakula cha hapa ambapo wanaamini wanaweza kufanyiwa hujuma.”