Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC Alberto Oliveira, ameanza tambo kuelekea Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kupangwa Droo ya Makundi ya Michuano hiyo.
Vipers SC itakayoshiriki kwa mara ya kwanza hatua hiyo, ikipangwa Kundi C lenye timu za Simba SC (Tanzania), Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco).
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema wameliona Kundi C na kukiri timu zilizpangwa kwenye Kundi hilo zina uzoefu wa utosha, lakini akasisitiza kikosi chake kitakuwa makini na kitapambana kwa dhamira ya kushinda michezo yote ya nyumbani na ugenini.
Amesema kikosi chake kimekuwa na wachezaji wenye kujiamini wakati wote hasa wanapocheza Michezo ya Kimataifa, na hiyo imekuja baada ya kuwang’oa waliowahi kuwa Mabingwa wa Afrika TP Mazembe ya DR Congo katika hatua ya awali.
“Nakiandaa kikosi changu na tuna muda wa kufanya hivyo, imani yangu tutafuzu kwenda hatua nyingine na mimi huwa napenda michezo mikubwa na yenye ushindani, iwe ndani au nje ya hapa (Uganda),”
“Wachezaji wangu wapo tayari kupambana kwenye Michezo ya namna hiyo, unafahamu tuliwatoa TP Mazembe ambayo imekua tishio katika Bara la Afrikwa kwa muda mrefu sana, hali hiyo iliwaongezea kujiamini Wachezaji wangu na sasa wanaona ni jambo la kawaida kuwa kwenye Michuano Mikubwa ya Bara hili.”
“Tuna muda kuiandaa timu kwa ajili ya kufuzu hatua inayofuata nina furaha na kikosi changu kutokana na kufanya vizuri na naamini watafanya vizuri pia kwenye nafasi ya makundi na kuipambania timu iweze kutinga hatua inayofuata,” amesema Alberto.
Vipers SC itaanza Kampeni ya kufuzu Hatua ya Robo Fainali ikitokea Hatua ya Makundi, kwa kucheza dhidi ya Raja Casablanca ugenini (Morocco), kabla ya kurejea nyumbani Uganda kupapatuana na AC Horoya ya Guinea.
Mchezo watatu kwa wababe hao wa Uganda utashuhudia ukirindima Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam dhidi ya Simba SC ya Tanzania, kabla ya timu hizo kucheza mchezo wanne nchini Uganda.
Mchezo watano kwa Vipers SC utakwa dhidi ya Raja Casablanca na mwisho watasafiri kuelekea Guinea kupapatuana na AC Horoya.