Kocha wa Viungo wa Simba SC Sbai Karim amefunguka kwa mara ya Kwanza tangu alipoajiriwa Klabuni hapo mapema mwezi huu, kwa pendekezo la Kocha Mkuu Zoran Maki.
Karim ambaye pia ni Kocha Msaidizi, amesema amefurahishwa na hatua ya kujiunga na Simba SC, kutokana na klabu hiyo kuwa na sifa za kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema jukumu kubwa alilonalo kwa sasa ni kuhakikisha wachezaji wanarejesha utimamu wao wa mwili, tayari kwa msimu mpya wa 2022/23, ambao anaamini utakua na upinzani mkubwa.
Amesema tangu alipoanza kazi Simba SC, amekua na uhusiano mzuri na kila mmoja aliyemkuta Kambini Ismailia, na upande wa wachezaji wanafurahishwa na mazoezi yake.
“Nimefurahi kuwa hapa, Simba SC ni klabu kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, nipo hapa kuhakikisha wachezaji wanakua timamu kimwili wakati wote, ni jukumu zito lakini nimeshaanza kazi na nimeona kila mmoja anafurahia tunachokifanya.”
“Simba SC ni klabu yenye mashabiki wengi, wana matarajio makubwa sana na timu yao kwa msimu ujao, hivyo sisi wahusika wa Benchi la Ufundi tutahakikisha tunapambana ili kufanikisha lengo la kuwafurahisha.”
“Wachezaji wote wa Simba SC wana uwezo mzuri na mkubwa, ndio maana kwa miaka ya hivi karibuni wamekua wanaifikisha klabu hii katika hatua za juu kwenye michuano ya Kimataifa, waliosajiliwa kwa sasa na hata wale waliokuwepo wana jambo kubwa sana, kwa sababu kuna jambo la kufanya ili kutwaa mataji msimu ujao.” amesema Sbai Karim
Kocha Sbai aliwahi kufanya kazi na Zoran Maki kwenye timu nyingi alizofundisha huko nyuma.
Zoran anavutiwa zaidi na kocha huyo wa viungo kwani mbali ya uwezo wake huo amekuwa pia akimsaidia kama kocha msaidizi ndio maana kila anapokwenda kufundisha anakuwa pamoja naye.