Picha mpya zilizopigwa kwa kutumia Satellite zimebaini kuwa Korea Kaskazini inajenga tena vinu vya makombora ya nyuklia, siku chache baada ya mkutano kati ya kiongozi wake Kim Jong Un na Rais wa Marekani, Donald Trump kuvunjika.
Kwa mujibu wa taarifa za wachambuzi ambazo zimeripotiwa na shirika la habari la Reuters, vinu hivyo vimeonekana katika eneo la Tongchang-ri ambalo lilikuwa likitumika kuzindua na kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia.
Kazi ya kuteketeza vinu hivyo ilianza mwaka jana, lakini ilisitishwa tena baada ya mazungumzo kati ya nchi hizo kuanza kuwa na muenendo usioridhisha.
Hivi karibuni, Marekani imeonya kuwa Korea Kaskazini inaweza kukabiliwa na vikwazo zaidi endapo itajaribu kuendeleza uundwaji wa silaha za kinyuklia.
Uthibitisho wa picha za satellite umewekwa wazi na wataalam wa intelijensia kutoka Korea Kusini ambao wamedai kuwa huenda kuna ukuaji wa haraka wa uzalishaji mpya wa roketi za makombora na mabomu ya nyuklia katika kituo hicho.
Kikao kati ya Trump na Kim Jong Un kilivunjika kwa kile ambacho Rais huyo wa Marekani alidai kuwa walitaka kuondolewa vikwazo vyote kama sharti la kuteketeza vinu vya silaha za nyuklia, lakini Marekani haikuwa tayari.