Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Simba SC, Suleiman Kova ameendelea kutoa ufafanuzi wa sakata la kiungo mkabaji wa klabu hiyo Jonas Mkude, ambaye anakabiliwa na tuhuma za utovu wa nidhamu klabuni hapo.
Kova ametoa ufafanuzi wa sakata la kiungo huyo, kufuatia baadhi ya mashabiki na wanachama wa Simba SC, kudai huenda Mkude anafanya makusudi kwa kuonesha utovu wa nidhamu mara kwa mara, kutokana na mkataba wake kufikia ukingoni.
Afisa huyo mstaafu wa jeshi la Polisi Tanzania, amesema Mkude bado ana mkataba mrefu na klabu ya Simba SC, hivyo amewataka mashabiki na wanachama kuwa watulivu na kuiachia kamati yake kufanya kazi.
Amesema kamati yake inafuata kanuni na sheria za klabu ya Simba SC zinazohusu nidhamu, hivyo kila kitu kitakwenda vizuri hadi mwisho wa sakata hilo ambalo limechukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari.
“Kuna watu nimeskia katika maoni yao wanafikiria labda mkataba wa Mkude unakaribia kuisha kwa hiyo Simba SC au sisi tunatumika kumkomoa mchezaji.”
“Nimeangalia mkataba wa Mkude bado ni mbichi kabisa, ni mchezaji anayependwa na kila Mwanasimba lakini linapotokea tatizo ni lazima lishughukikiwe.” Suleiman Kova.
Kamati ya Nidhamu ya Simba SC inaendelea kususbiri majibu ya vipimo vya Jonas Mkude, baada ya kuagiza mchezaji huyo akapimwe akili, ili kufahamu anasumbuliwa na tatizo gani, hadi kufikia hatua ya kufanya mambo ambayo si rafiki ndani ya klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.