Kasi ya Rais John Magufuli ya kubana matumizi ya serikali imegeuka kilio kwa wafanyabiashara wengi na wanasiasa mjini Dodoma ambako vikao vya Bunge la Bajeti vinaanza mapema leo.

Mpango huo wa kubana matumizi umepelekea magari aina ya mashangingi na idadi kubwa ya watu waliofika na misafara ya vigogo mjini humo kuwa historia, hali iliyozitafuna biashara zilizozoeleka kufana wakati wa vikao vya Bunge mjini humo.

Wafanyabiashara hao wamelalamikia kudorola kwa biashara za nyumba za kulala wageni, kumbi za starehe, kumbi za mikutano, biashara ya magari ya kukodi au taxi pamoja na biashara ndogondogo zilizokuwa zinanunuliwa na baadhi ya watu waliowasindikiza ‘waheshimiwa’. Kwa kawaida Bunge lilikuwa linaenda na neema kwa wafanyabiashara mjini humo.

Baadhi ya Wizara tayari zimeweka msimamo wake kuhusu kupunguza idadi ya maafisa watakaofika Bungeni kwa ajili ya kufuatilia bajeti za wizara husika tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Lazima tuangalie umuhimu wa mtu kulingana na sekta yetu ya elimu hatutaweza kuja na watu kama ilivyozoeleka huko nyuma,” Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako anakaririwa.

Kadhalika, idadi ya watu wa kawaida waliokuwa wakifika katika mji huo wakati wa vikao vya Bunge imepungua kwa kiasi kikubwa katika siku mbili zilizoshuhudiwa kabla ya kufikia leo ambapo Bunge linaanza.

Hii inawakumbusha kauli ya Rais Magufuli wakati wa kampeni akiwaomba kura wananchi, “mimi si ndio Magufuli, nichagueni nikawafunge makufuli kama lilivyo jina langu.”

Sasa ameendelea kufunga makufuli mianya yote ya matumizi yasio ya lazima yanayoligharimu taifa ili pesa zielekezwe kwa wananchi.

Video: Rais Magufuli amuapisha Balozi Chikawe
Mzee Yusuf asema neno kwa Diamond na Ali Kiba, ‘wanaume hawanuniani’