Maafisa waandamizi wa Taliban na wawakilishi wa Marekani wamekutana nchini Qatar kujadili jinsi ya kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Afghanistan na taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani.
Maafisa wa nchi hizo mbili wamejifungia jijini Doha kujadili ana kwa ana, ikiwa ni mkutano wao wa kwanza tangu Marekani ilipoondoa vikosi vyake vya kijeshi nchini Afghanistan Agosti mwaka huu, ikiwa ni miaka 20 tangu walipoingia kijeshi nchini humo.
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, Mullah Amir Khan Muttaqi amewaambia waandishi wa habari kuwa majadiliano yalihusu zaidi msaada wa kibinadamu pamoja na namna ya kutekeleza makubailiano waliyotiliana sahihi jijini Washington mwaka jana, ambayo yalisababisha Marekani kukamilisha hatua ya kuondoa vikosi vyake.
Waziri huyo amesema kuwa wawakilishi wa Afghanistan wameiomba Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Benki Kuu ya Afghanistan. Pia, amesema Marekani itatoa msaada wa chanjo ya UVIKO-19 kwa raia wa Afghanistan.
Taliban wanaendelea kutafuta kuungwa mkono na dunia, ambapo baada ya kikao hicho wanatarajia kukutana na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya.
Wapiganaji wa Taliban waliondolewa katika utawala wa Afhganistan miaka 20 iliyopita, baada ya Marekani kuvamia nchi hiyo wakimtafuta Osama Bin Laden na Al-Qaeda. Mwaka huu, Marekani iliondoa vikosi vyake na Taliban wakafanikiwa kurejea tena madarakani kwa makubaliano maalum.