Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa amewataka watumishi wa umma kutotumia simu binafsi wakiwa ofisini wakati wanawahudumia wananchi.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa mkoani Simiyu mwisho mwa juma, alipokuwa katika mkoa huo kwa lengo la kuhimiza utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Waziri Mchengerwa amesema kuwa watumishi wenye tabia hizo huwakatisha tamaa wananchi wanaopata huduma katika maeneo yao ya kazi, kwakuwa wanajali zaidi simu zao kuliko kutoa huduma husika kwa wakati.

“Kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia simu, na hata wakiwaona wateja wamekuwa wakiendelea kufanya hivyo badala ya kutoa huduma. Ninawataka muache tabia hiyo mara moja,” alisema Waziri Mchengerwa.

“Tufanye kazi kwa weledi, kujitoa na kuwasilikiza wananchi wanapofuata huduma. Tuwajali kwa maana nchi hii ni ya kwao na tupo kwa ajili yao,” aliongeza.

Aidha, Waziri huyo alionya kuhusu mavazi yasiyofaa yanayovaliwa na baadhi ya watumishi wa umma wawapo ofisini.

Amewataka watumishi kuzingatia waraka wa utumishi wa umma Na. 6 wa mwaka 2020 unaotoa maelekezo ya mavazi katika ofisi za umma.

Kuna jambo: Taliban, Marekani wajifungia Qatar
Uzinduzi wa kampeni ya maendeleo na mapambano dhidi ya Uviko 19