Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka Ukanda ya Maziwa Makuu wamekutana nchini Uganda kupanga mikakati ya kukabiliana na tishio la kundi la Islamic State ambalo limeripotiwa kuanza kuendesha harakati zake katika maeneo ya Mashariki na Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hayo ni kwa mujibu wa Upelelezi wa chombo cha usalama kinachowaleta pamoja wakuu wa usalama katika kanda ya maziwa makuu, ambapo kimesema kuwa kuna uwezekano wa eneo hilo kuingiliwa kirahisi na wanamgambo wa kundi hilo kutokana na ukosefu wa usalama na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Vyombo vya ulinzi na usalama katika eneo hilo vinataka kuhakikisha kuwa kundi hilo halipati nafasi ya kuendesha shughuli zake katika matatifa ya eneo hilo baada ya kutimuliwa Mashariki ya Kati.
”Kuna vitisho katika ukanda wetu, kwa hiyo ni onyo kwetu kulishughulika mapema kabla halijawa tatizo kubwa katika kanda ya maziwa makuu,”amesema Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali David Muhoozi’
Aidha, kulingana na wakuu hao wa ulinzi na usalama wamesema kuwa kuna haja ya wao kushirikiana na majeshi ya mataifa ya kigeni yaliyochangia katika juhudi za kuvunja kundi hilo mashariki ya kati.
Hivi karibuni kundi la kigaidi la Islamic State ambalo chimbuko lake ni nchini Iraq, lilidai kufanya mashambulizi katika kijiji cha Kamango mkoani Kivu Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.