Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Seleman Zedi amesema Halamshauri ya wilaya ya Biharamulo haikuwa tayari kushiriki kikao ambacho kiliwataka kutoa maelezo ya utekelazaji wa maagizo 33 yaliyotolewa kwao na kamati hiyo.
Zedi ameyasema hayo Jumatano Agosti 31, 2022 wakati wa uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2021.
“Sisi kama kamati, utekelezaji wa maagizo tunaona kama utii wa kamati, sasa ukichukulia kama walipewa maagizo 33 wakatekeleza 3 ni asilimia ndogo sana. Wengi wanaokuja hapa wanakuwa hawajatekeleza maagizo yote ila watakuwa wamevuka walau asilimia 50, sasa hao wanakuja hapa na sababu ambazo hazina mashiko,”
Ameongeza kuwa Viongozi hao walisema, “walikuwa na Mkurugenzi mpya lakini ukiangalia Mkurugenzi huyo alikuwa na zaidi ya Mwaka kwa sababu alifika pale mwaka jana Agosti, na Halmashauri nyingine ambazo zimefika hapa na zenyewe zina wakurugenzi wapya lakini wamefanikiwa kutekeleza maagizo.” amesema Zedi.
LAAC ililazimika kuwaondoa katika kikao hicho viongozi wa Halamashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera baada ya kutekeleza maagizo matatu kati ya 33 waliyowapatia miaka iliyopita.