Serikali inapanga kuwafunga vinasa mawimbi maalum (collar), Tembo viongozi ili kufuatilia mienendo ya uelekeo wa makundi yao kwa ajili ya kuwadhibiti pindi wanapoelekea katika makazi ya wananchi

Sambamba na hatua hiyo, pia Serikali inapanga kuendelea na zoezi la uelimishaji kwa wananchi juu ya mbinu mbalimbali za kukabiliana wanyama wakali na waharibifu ili kuepusha madhara yambayo yamekuwa yakijitokeza.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Bungeni jijini Dodoma.

Amesema, “Serikali ina mikakati ya kupunguza changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuongeza idadi ya askari wa uhifadhi na kuwepo kwa namba maalum ambazo wananchi watapiga bure ili kutoa taarifa wanapovamiwa na wanyama wakali.”

Ameongeza kuwa, Wizara itaendelea kujenga mahusiano mazuri na Halmashauri za Wilaya, ili kusaidia kupunguza changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hasa jamii ya Tembo na kuwaomba wabunge kuelimisha wananchi kuacha ukinzani na sheria za uhifadhi.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Juma Ally Makoa ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ili kuimarisha mbinu za kudhibiti tembo.

Baadhi ya watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakifuatilia mada zinazowasilishwa wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Bungeni jijini Dodoma.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Eliamani Sedoyeka amewataka Wabunge kuendelea kuwashawishi wananchi kupanda miti na kutumia nishati mbadala ili kulinda kulinda uhifadhi na mazingira.

Vikao vya Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi ,Maliasili na Utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii vinaendelea kwa lengo la kujua utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya Wizara.

LAAC:Biharamulo hawakuwa tayari kukaguliwa
Habari kuu kwenye magazeti ya leo September 1, 2022