Klabu za Liverpool, Bayern Munich na Paris St-Germain zipo kwenye vita kali ya kuiwania huduma ya kiungo mkabaji wa PSV Eindhoven lbrahim Sangare mwenye umri wa miaka 25 kwenye dirisha hili.
Liverpool imelazimika kutua kwa Sangare baada ya kuachana na dili la kiungo wa Brighton, Moises Caceido ambaye amekataa kutua Anfield.
Sangare ni aina ya kiungo ambaye Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp huwa anawahitaji.
Inadaiwa Liverpool, Bayern Munich ziko tayari kutoa dau la Pauni 32 Milioni ili kuinasa saini ya nyota huyo wa kimataifa wa lvory Coast.
Hata hivyo, hivi karibuni PSV inadaiwa kukataa ofa ya Nottingham Forest iliyokuwa inamhitaji Sangare kwa mkopo.
PSV inadaiwa kuhitaji zaidi ya Pauni 32 Milioni ili kumuuza Sangare.
Notingham iliwasilisha ofa hiyo ikiwa inaamini kwamba kwenye mkataba wa Sangare kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayomhitaji itatoa kiasi hicho cha pesa.
Sangare ni miongoni mwa mastaa waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Uholanzi kwa msimu uliopita ambapo alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao manane.
Wakala wa staa huyu amethibitisha timu zote hizo tatu bado zipo kwenye mazungumzo na PSV kuhusiana na masuala ya ada ya uhamisho. Mkataba wa sasa wa kiungo huyo unatarajiwa kumalizika mwaka 2025.