Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Leandro Trossard anatarajiwa kufanyiwa vipimo leo Ijumaa (Januari 20) jijini London, baada ya kufikia makubaliano binafsi na Klabu ya Arsenal.
Trossard anatarajiwa kujiunga na Arsenal, akitokea BrighBrighton & Hove Albion, ambayo imekubali kumuuza kwa thamani ya Pauni Milioni 27, baada ya kuwa na mazungumzo na Uongozi wa Arsenal iliyowasilisha ofa yao tangu mwanzoni mwa juma hili.
Brighton & Hove Albion imefikia maamuzi ya kumuuza Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, kufuatia kushindwa kumshawishi kusaini mkataba mpya, kufuatia ule wa awali kusaliwa na muda miezi sita klabuni hapo.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa Trossard, alifikia hatua ya kugomea mazoezi ya kikosi cha Brighton & Hove Albion, ili kushinikiza usajili wake wa kwenda jijini London kujiunga na Arsenal.
Awali Mshambuliaji huyo aliwaniwa na Klabu ya Tottenham Hostspurs, lakini ofa ya klabu hiyo ilikataliwa kwa misingi ya kumshinikiza Trossard kuendelea kubaki Falmer Stadium.
Arsenal ilihamishia nguvu ya kumsajili Trossard, baada ya kushindwa kumnasa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ukraine Mykhailo Petrovych Mudryk, aliyetimkia Chelsea akitokea Shakhtar Donetsk kwa ada ya Pauni milioni 85.
Hata hivyo tangu mwaka 2019 Mykhailo Mudryk alitolewa kwa mkopo katika klabu za Arsenal Kyiv (2019) na Desna Chernihiv (2020).