Klabu ya Leicester City wanatarajia kuvuna hadi Pauni 200 milioni kwenye mauzo ya mastaa endapo kama watashuka daraja kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Leicester City imejiweka kwenye hatari ya kucheza Championship msimu ujao baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Liverpool. Timu hiyo imebakiza mechi mbili dhidi ya Newcastle United na West Ham United.
Lakini, kama watashindwa kubaki Ligi Kuu England na kushuka daraja, basi wanaweza kuvuna hadi Pauni 200 milioni kwenye makusanyo ya mauzo ya wakali wao matata.
James Maddison ni mmoją wa mastaa watakaouzwa, huku akitajwa kuwa na thamani ya Pauni 48 milioni.
Newcastle, Manchester United na Tottenham zinahitaji saini yake, ambapo kwa msimu huu amefunga mabao 10 na asisti tisa katika mechi 28.
Staa mwingine ni Harvey Barnes anayethaminishwa kwa Pauni 28 milioni, huku naye akiwa amefunga mabao 12 msimu huu.
Kiungo Youri Tielemans naye ataondoka na mchezaji huyo thamani yake ni Pauni 26 milioni.
Pacha wawili kwenye kiungo, Wilfred Ndidi na Boubakary Soumare nao watakuwa kwenye orodha hiyo, huku thamani yao ya pamoja ikiwa Pauni 45 milioni.
Mabeki wa pembeni Ricardo Pereira na Timothy Castagne ambao thamani yao ni Pauni 24 milioni, watakuwa kwenye orodha ya wanaoweza kuuzwa na beki wa kati, Caglar Soyuncu.
Thamani ya beki huyo Mturuki ni Pauni 13 milioni na kama vote watauzwa, basi Leicester City itakwenda kwenye Championship ikiwa na pesa ndefu, Pauni 200 milioni.