Mshambuliaji kutoka DR Congo na Klabu ya Young Africans Fiston Mayele amechimba mkwara mzito kuelekea mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ambapo watakutana na USMA ya Argeria mwishoni mwa juma lijalo jijini Dar es salaam, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mshambuliaji huyo ambaye amekuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Young Africans tangu aliposajiliwa mwishoni mwa msimu wa 2020/21, amesema ukiachana na malengo ya timu kushinda ubingwa wa michuano hiyo, atapambana kufunga bao kwenye fainali ili kutimiza malengo ya kushinda tuzo ya kiatu cha mfungaji bora.

Mayele juzi Jumatano (Mei 17) alikuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Marumo Gallants baada ya kuhusika kwenye mabao mawili akifunga bao moja na kuasisti moja wakati Yanga ikiwaondosha Marumo kwenye mchezo wa nusu fainali ya mashindano hayo uliopigwa kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Royal Bafokeng.

Bao hilo limemfanya Mayele kufikisha mabao sita akiongoza msimamo wa wafungaji sambamba na mpinzani wake mkubwa Ranga Piniel Chivaviro wa Marumo Gallants ambaye naye alifunga bao la kufutia machozi la Marumo kwenye mchezo huo.

Mayele amesema: “Jambo la msingi kwa sasa ni kufanikisha malengo ya kucheza fainali, lakini kama mchezaji binafsi ukiachana na kujitoa kuisaidia timu kushinda ubingwa huu natamani kuona nashinda pia tuzo ya ufungaji bora.

“Nafahamu tunauendea mchezo mgumu, lakini nitapambana kufunga bao kwenye fainali ikiwa nitapewa nafasi ili kuisaidia Yanga kushinda ubingwa na kufikia malengo yangu ya kushinda tuzo ya mfungaji bora.”

Baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza hatua ya Fainali, Young Africans itakwenda Algeria kwa mchezo wa Mkondo wa Pili ambao umepangwa kupigwa Juni 03, katika Uwanja wa Omar Hammadi.

Leicester City kuvuna Pauni Milion 200 England
Mke roboti kupunguzia gharama za maisha - Elon Musk