Mgombea ubunge wa jimbo la Kahama Mjini kwa tiketi ya Chadema, James Lembeli amedai kuwashangazwa na kauli za baadhi ya viongozi na wagombea ubunge kupitia CCM waliomzushia maafa na umahututi kufuatia ajali ya gari aliyoipata hivi karibuni.

Akiongea na waandishi wabari jana nyumbani kwake (Kahama), Lembeli alieleza kuwa amesikitishwa na kauli za wagombea hao na kuwaeleza kuwa walichokifanya sio jambo la kiungwana.

“Ndugu zangu wa Chama Cha Mapinduzi, na hasa viongozi au wagombea katika jimbo la Msalala, kunitangazia mimi katika mikutano ya kampeni kwamba ‘jimbo la Kahama sasa liko wazi kwa sababu Lembeli hivi sasa amepata ajali na yuko mahututi’, si jambo jema na sio uungwana. Kufurahia maumivu ya mwenzio au kifo cha mwenzio si jambo la kheri,”

Hata hivyo, Mgombea huyo alikiri kuwa alipata ajali mbaya ya gari iliyopelekea gari kupinduka wakati wakiwa safarini kutoka Simanjiro wakielekea Arusha baada ya kuacha njia lakini abiria wote pamoja na dereva walinusurika na hawakupata majeraha kama ilivyodaiwa.

Alieleza kuwa ndani ya gari hilo alikuwa pamoja na mbunge aliyemaliza muda wake, Joyce Mukya ambao wote wako salama.

“Kuhusu kile kinachoendelea katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habri mbalimbali sio kweli, mimi sijaumia na wala sikuwa mahututi na wala sina hali mbaya. Kwahiyo niwaombe ndugu zangu wa Wilaya ya Kahama kwa ujumla kwamba msiwe na wasiwasi, Lembeli nipo na kwa wana Chadema haya yalikuwa ni majaribu na ni ishara ya ushindi tosha.” Aliongeza.

Kuhusu Kufungwa Rasmi Uchumi ‘Supermakets’ Tanzania, Uganda
John Bocco Atuma Salamu Jangwani