Bingwa wa zamani wa masumbwi ya uzito wa juu, Lennox Lewis ameonesha kuchoshwa na tambo za maneno kati ya wababe ambao hawajawahi kupigwa, Anthony Joshua na Deontay Wilder, na kuwataka ‘waache maneno waweke muziki’.
Hatua hiyo ya Lewis imekuja baada ya kushindwa kufanyika kwa pambano la wababe hao mwaka huu licha ya kuwepo mazungumzo yaliyochukua zaidi ya mwaka mmoja yakiambatana na tambo za pande zote.
Wiki iliyopita, kambi ya A. Joshua iliweka wazi kuwa pambano hilo halitakuwepo ikiwarushia lawama kambi ya Wilder, ambayo nayo ilirejesha lawama hizo. Kambi ya Joshua (21-0) imesaini mkataba wa pambano la mwezi Septemba dhidi ya mbabe mwingine, Alexander Povetkin (34-1).
Hatua hiyo inafanya ndoto ya kuwepo pambano kati ya Joshua na Wilder mwaka huu kuyeyuka, huenda hadi Aprili mwakani.
Lewis ambaye ana rekodi nzito kwenye mchezo huo akiwa ‘undisputed champion’ aliyezima kabisa ubabe wa Mike Tyson na Evander Holyfield, amesema kuwa amechoshwa na kurushiana maneno kwa wababe hao kwa miaka miwili na kwamba ingekuwa enzi zake vitendo vingeongea.
“Nilipokuwa bingwa, nilikuwa nataka kupambana na bondia bora ili kuonesha dunia nani ni bora zaidi, basi,” alitweet Lewis. “Nimekuwa nasikia wakizungumzia pambano hilo, lakini nimeona AJ (Joshua) akibadili mawazo… kama pande zote wangetaka pambano hili, lingekuwa limefanyika. Mwisho wa simulizi,” ameongeza.
Pambano kati ya Joshua na Wilder litakuwa ni pambano linalosubiriwa kwa hamu zaidi duniani kwenye uzito wa juu, katika kipindi cha miaka 15.