Udumavu katika Mkoa wa Iringa bado ni tatizo kubwa licha ya Mkoa huo kuwa wazalishaji wa chakula na kutegemewa nchi nzima, ambapo utafiti wa Tanzania Demographic Health Survay (TDHS) wa mwaka 2018, unaonesha asilimia 31.8 ya watoto walidumaa.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo hii leo Mei 27,2023 Wilayani Mafinga Mkoani Iringa, wakati akizungumza na wananchi wa shina namba 3 kata ya Boma katika ziara yake ya kuimarisha chama.
Amesema, Mkoa wa Iringa unaongoza kwa kuwa na udumavu kwa kuwa 59. 9, Njombe asimia 50.4 na Rukwa ni 49.8 na hivyo kuwataka wazazi, viongozi na makundi mbalimbali ya kijamii kuhamasisha ulaji wa chakula bora ili kuondoa tatizo hilo.
“Nawaomba wazazi mzingatie malezi bora ya watoto na lishe bora ili watoto waweze kuwa na afya bora na malezi sahihi katika jamii kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia watoto kuwa na akili,” amesema Chongolo.
Aidha, ameongeza kuwa chakula na lishe bora ndio inayotengeneza akili ni muhimu watoto kupata elimu bora na kuwawekea utaratibu wa kujiendeleza pindi wanapomaliza shule ili waweze kujiajiri na sio kuishia mtaani.
Amewakumbusha viongozi wa mkoa huo kuendelea kutoa elimu kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kuwa Iring takwimu zinaonyesha bado maambukizi yako juu.
Ziara ya Katibu mkuu huyo wa CCM inaendelea mkoani Iringa akiwa ameambatana na Katibu NEC itikadi na Uenezi, Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC Oganaizesheni, Issa Haji Gavu.