Kikosi cha Timu ya Manispaa ya Kinondoni, KMC FC mapema hii leo kiliwasili jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wa mzunguko wa nane dhidi ya Young Africans utakaopigwa Jumapili, Oktoba 25 kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Kikosi cha KMC FC kiliondoka jijini Dar es Salaam saa 12.00 asubuhi kwa usafiri wa Ndege ya Air Tazania kikiwa na wachezaji 30, Viongozi pamoja na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Habibu Kondo na kuwasili jijini Mwanza saa 1.30 asubuhi.
Mkuu wa Idara Ya Habari Na Mwasiliano ya klabu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam Christia Mwagala, amesema baada ya kuwasili jijini humo, kikosi chao kinaendelea vizuri na kitaendelea na maandalizi kabla ya kuwakabili Young Africans Jumapili, Oktoba 25.
“Kwa ujumla benchi la ufundi likiongozwa na Kocha msaidizi wa timu hiyo Habibu Kondo ambaye ameungana na kikosi hicho, leo hii wanafanya maandaalizi ya kuhakikisha kwamba KMC FC inakwenda kufanya vizuri katika michezo hiyo mitatu ikiwemo huo wa Young Africans.” Amesema Christia Mwagala
Mbali na maandalizi ya mchezo huo, KMC FC pia inajiandaa kucheza na Timu ya Gwambina katika Uwanja wa Gwambina Oktoba 30 mwaka huu pamoja na Biashara United Mara katika Uwanja wa Karume mjini Musoma Mkoani Mara.
Hadi sasa KMC FC imecheza michezo saba na kushinda mitatu, huku ikitoa zare michezo miwili na kufungwa michezo miwili na kwamba imejipanga katika kuhakikisha kuwa inavuna alama zote tisa katika michezo mitatu ya hivi sasa.