Uongozi wa klabu ya Manchester United umepongezwa kwa kuchukua hatua ya kuzipunguza mwanga baadhi ya herufi za maandishi kwenye neno Manchester lililoandikwa uwanja wa Old Trafford na kubakia herufi NHS UNITED.
Uongozi wa Manchester United umechukua hatua hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wafanyakazi wanaopambana na virusi vya Corona.
Pongezi hizo zimetolewa na magwili wa soka la England Gary Lineker na Gary Neville kwa kusema inapendeza na kutia moyo kwa mashabiki wa klabu hiyo, ambao pia wameungana na watu wote duniani kupambana na Virusi vya Corona.
Wawili hao wamesema Manchester United ni klabu kubwa na maamuzi yaliyochukuliwa na uongozi wake, yanadhihirisha ni vipi walivyoguswa na tatizo linaloendelea kuiandama dunia kwa sasa.
Maeneo mengine nje ya uwanja wa Old Trafford, yamewashwa taa za bluu ili ziendane na rangi ya mfumo wa huduma ya afya nchini England.
Man United, imesifiwa kwa namna inavyounga mkono mapambano dhidi ya virusi vya Corona, ambapo imetoa msaada wa kifedha katika huduma za afya kutoka Taasisi yake ya Manchester United na vilevile imetoa magari ya kusaidia shughuli za kila siku za wahudumu wa afya.