Baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa nyumbani, leo Lipuli FC inashuka kwenye dimba la ugenini, Sokoine jijini Mbeya kuikabili Mbeya City katika mchezo wa kwanza wa raundi ya 14 ya ligi hiyo.

Lipuli imetoka kupokea vipigo mfululizo kutoka kwa Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar, huku Mbeya City ikitoka kupoteza katika uwanja huo dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo uliopita hivyo timu zote zitahitaji ushindi ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi, Mbeya City ikiwa nafasi ya 13 na pointi 12 wakati Lipuli ikiwa nafasi ya nane na pointi 14.

Mchezo mwingine uliokuwa umepangwa kupigwa leo kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza kati ya Mbao FC ya Mwanza na Stand United  ya Shinyanga, umesogezwa mbele hadi kesho Jumamosi kufuatia mabadiliko ya ratiba ya uwanja ambao utatumika kwa shughuli za kiserikali.

Katibu wa Chama cha Soka mkoani Mwanza, Leonard Malongo licha ya kubainisha mabadiliko ya ratiba hiyo amesema hatua hiyo ichukuliwe kama fursa ya mandalizi  kwa timu hizo.

Kwa maana hiyo, kesho kutapigwa jumla ya michezo miwili ambapo michezo mwingine utazikutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Njombe Mji, mchezo ukipigwa dimba la Manungu Morogoro.

Jumapili kutakuwa na michezo miwili, ambapo mabingwa watetezi, Yanga watakuwa katika dimba la Taifa Dar es Salaam kupambana na Ruvu Shooting huku Azam wakiwa Jijini Mbeya kuwavaa maafande wa Tanzania Prisons.

Toronto Raptors yazidi kuifukuzia Boston
Sanchez aondolewa mazoezini Arsenal