Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, leo Agosti 26, 2019 ameshinda pingamizi la Serikali, dhidi ya maombi ya kibali cha kufungua kesi kupinga kuvuliwa ubunge na Spika wa Bunge Job Ndugai.
Kesi hiyo ya maombi namba 18 ya mwaka 2019, ilifika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, leo kwa ajili ya kutolewa maamuzi ya maombi yaliyowasilishwa na Mbunge huyo, kama yana sifa ya kusikilizwa mahakamani hapo, ambapo Mahakama Kuu imekubali kusikiliza ombi lake.
Aidha, kutokana na hatua hiyo, maombi ya Lissu ya kutetea Ubunge wake wa Singida Mashariki yataendelea kusikilizwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Sirilius Matupa.
Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu aliiomba Mahakama hiyo, impe kibali cha kufungua kesi, ili Mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe Lissu taarifa yake ya kumvua Ubunge.
Katika maombi hayo, Lissu ameiomba Mahakama hiyo itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai, kumvua Ubunge pamoja na kuiomba Mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa Mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu