Mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewataka wananchi wa Kigoma mjini kuchagua kiongozi yeyote mwenye nguvu kati ya ACT- Wazalendo na CHADEMA.
Lissu, ameewaacha njia panda wanachama wa chama hicho katika jimbo la Kigoma Mjini wakati akizungumza katika kampeni ya kuomba ridhaa ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa Octoba 28, mwaka huu.
” Kama mgombea katika jimbo hili ana nguvu, mchagueni huyo na kama mgombea wa chama cha ACT – Wazalendo, ana nguvu muungeni mkono yeyote mwenye nguvu ndio mgombea wangu,” amesema Lissu.
Aidha, amesema kuwa lengo la upinzani ni kuing’oa CCM, hivyo uamuzi wa nani anapaswa kupewa kura kwenye jimbo hilo ameuacha kwenye mikono ya wakazi wa jimbo hilo.
Juzi Septemba 19, mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, akiwa katika kata ya Chiungutwa, Wilayani masasi , Mkoani Mtwara alimnadi Frank John, mgombea Udiwani wa kata hiyo kupitia CHADEMA.
” Tunachotaka ni kuhakikisha tunapata diwani wa upinzani hapa, inatakiwa mumpe kura, tunachokitaka ni kufanya kazi kwa maslahi ya watu sio maslahi ya vyama hivyo tunamuunga mkono huyu wa CHADEMA,” Alisema Zitto.