Majogoo wa jiji Liverpool wamekubali kutoa ada ya Pauni milioni 57.1, ili kukamilisha dili la usajili wa kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Nabil Fekir.
Taarifa zilizochapishwa na gazeti la L’Equipe la Ufaransa zimeeleza kuwa, kiungo huyo wa klabu ya Olympic Lyon anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya leo ijumaa.
Gazeti hilo limemnukuu rais wa Olympic Lyon Jean-Michel Aulas akisema kuna uwezekano wa uhamisho wa kiungo huyo kukamilishwa kabla ya kuanza kw afaianli za kombe la dunia.
“Uhamisho wake unatarajiwa kukamilika wakati wowote kabla ya kuanza kwa fainali za kombe la dunia, tulitarajia huenda dili hili lingekamilika baada ya fainali hizo kuchezwa.
“Wenzetu wameonyesha uharaka wa kutaka usajili wa Nabil Fekir, ufanyike kipindi hiki.”
Olympic Lyon waliwahi kutoa video na kuisambaza katika mitandao ya kijamii, ikieleza uhamisho wa Nabil Fekir hautofanyika kabla ya fainali za kombe la dunia.
Maamuzi hayo yalifanywa na uongozi wa klabu hiyo, kufuatia kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps kuweka msimamo wa kutomruhusu mchezaji huyo kuondoka kambini katika kipindi hiki cha maandalizi ya kombe la dunia.
Fekir mwenye umri wa miaka 24, alifunga mabao 23 msimu wa 2017/18 huku akitoa pasi za mwisho tisa.
Katika upande wa timu ya taifa Fekir alifungia bao lake la kwanza wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Ufaransa na Jamuhuri ya Ireland uliochezwa Mei 28.