Majogoo wa Jiji ‘Liverpool FC’ wamekubali kumsajili Mshambuliaji kutoka nchini Uholanzi na Klabu ya PSV Eindhoven, Cody Gakpo, baada ya kukaribishwa katika meza ya mazungumzo.
Gakpo mwenye umri wa miaka 23, alikuwa sehemu ya kikosi cha Uholanzi kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, na aliifungia timu hiyo mabao matatu.
Ada ya ya usajili wa Mshambuliaji huyo inatajwa kuwa kati ya Euro Milioni 40-50 sawa na Pauni Milioni 35.4 – 44.3.
Uongozi wa PSV umeeleza kuwa, Gakpo huenda akaanza safari ya kuelekea England kwa ajili ya kukamilisha dili la kujiunga na Liverpool sambamba na kufanyiwa vipimo vya afya.
Liverpool wamejitosa kwenye usajili wa Mshambuliaji huyo, kufuatia kuumia kwa Wachezaji Luis Diaz na Diogo Jota, ambao wote kwa pamoja huenda wakashindwa kurejea Uwanjani hadi mwishoni mwa msimu huu.
Klabu ya Manchester United nayo ilitajwa kumuwania Gakpo, lakini ilichelewa kuthibitisha kama ingeingia katika Dili la kuiwania saini ya Mshambuliaji huyo Kinda, na kuifanya Liverpool kupenya kwa urahisi.
Katika Ligi ya Uholanzi, Gakpo amekua na mwenendo mzuri msimu huu, kwani hadi sasa ameshafunga mabao Tisa na kutoa Asist Kumi na Mbili, katika Michezo 14 ya Ligi aliyochezwa hadi sasa.