Majogoo wa Jiji ‘Liverpool’ wametangaza rasmi kujiundoa katika harakati za kumsajili kiungo kutoka nchini England na Klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani Jude Bellingham.
Liverpool ilikuwa ikitajwa kujiandaa na mpango wa kumsajili Kiungo huyo wakati wa usajili wa Majira ya joto, na sasa imehamisha mpango huo kwa kutenga fedha kwa ajili ya kukifanyia marekebisho kikosi chao kinachonolewa na Meneja kutoka nchini Ujerumani, Jurgen Klopp.
Kwa muda mrefu The Reds ilikuwa ikihusishwa na tetesi za kuhitaji huduma ya Bellingham, lakini gharama ya uhamisho wake zimekuwa kikwazo na kuufanya Uongozi wa Klabu hiyo kubadili mawazo na kujiweka pembeni.
Klopp ameweka wazi hitaji la kikosi chake kufufuliwa wakati wa msimu mgumu ambao unawafanya kudorora katika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, huku akisaliwa na Michezo tisa msimu huu, akiwa nyuma kwa alama 12 kutoka nafasi nne za juu.
Kukosa kushiriki Ligi ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kunaweza kupunguza zaidi fedha zinazopatikana msimu huu wa joto na vile mvuto wao kwa walengwa wa kuhama.
Meneja wa Liverpool ameweka kipaumbele katika kuimarisha safu ya kiungo na wachezaji kadhaa wanaweza kuhitajika huku Alex Oxlade-Chamberlain, James Milner na Naby Keita wote wakiwa nje ya mkataba msimu huu wa joto.
Vyanzo viliiambia ESPN mwezi uliopita kwamba Manchester City walikuwa wanajiamini kwamba wanaweza kupata saini ya Bellingham, ingawa miamba wa Hispania, Real Madrid wanasalia kwenye mbio hizo.