Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameeleza jinsi ambavyo Rais John Pombe Magufuli ameweza kushinda vita dhidi ya kasi ya maambukizi ya virusi vya corona, licha ya kuwepo vitisho.
Akizungumza katika mkutano wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika jana katika jimbo la Monduli ambapo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda alikuwa mgeni rasmi, Lowassa alisema kuwa walimtia moyo Rais Magufuli dhidi ya vitisho hivyo.
“Kulikuwa na maneno mengi, fujo… fujo, wengine wanatisha, wanaonekana kwenye mitaa na wengine kwenye ma-TV, na Ma-TV mengine yanatishatisha. Lakini tulimwambia rais wetu usitishike hata kidogo. Umma wa Watanzania uko nyuma yako na dunia inajua kwamba kuna mwanaume Tanzania,” amesema Lowassa.
Ameeleza kuwa katika vita dhidi ya virusi vya corona, kuna baadhi ya marais wa nchi kama Australia na Bolivia wamelazimika kujiuzulu, lakini hali ilikuwa tofauti kwa Tanzania kwa jinsi ambavyo Rais Magufuli alimtanguliza Mwenyezi Mungu na kuishangaza dunia.
“Ninyi mtu wenu tena mweusi, hana nguvu za kiuchumi au kiutume anawaambia tumuendee Mwenyezi Mungu tumuombe atusaidie tuondokane na hili janga. Na watu wa ajabu, wakasema huyu anababaisha tu… lakini tumepita wiki mbili, wiki tatu, hakuna corona,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Lowassa alisema kuwa ana uhakika Rais Magufuli atashinda tena katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, lakini ambacho hakifahamu ni idadi ya kura ambazo zitampa ushindi huo.
Lowassa na Pinda waliwasihi wanachama wa chama hicho kumuunga mkono kwa kishindo Rais Magufuli kumuombea kura nyingi kwa wananchi, pamoja na kumuombea kura mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho kwenye jimbo hilo, Fred Lowassa.