Hatimaye viongozi waandamizi wa Chadema jana waliungana na mamia ya wafuasi wa chama hicho pamoja na familia ya Marehemu Alphonce Mawazo kutoa heshima zao za mwisho katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza baada ya kuruhusiwa na Mahamaka.

Akiongea kwa majonzi wakati wa tukio hilo, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliwataka polisi kuacha kukandamiza haki za watu kwa kufuata kile alichodai ni ‘utawala wa imla’.

“Hawa Polisi wanafanya mambo yao kiimla-imla, kiujanja ujanja, wao wameleta magari ya washawasha yaliyonunuliwa kwa Dola za Kimarekani 282 milioni, hawana namna ya kuyatumia, wameamua kuwachokoza wananchi ili waweze kuyatumia,” alisema Lowassa na kuwataka wananchi kuwa watulivu ili polisi washindwe kuyatumia magari hayo.

Lowassa ambaye amsifia Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Mlacha aliyetoa uamuzi wa mwili wa marehemu Mawazo kuagwa jijini humo, aliwataka polisi kuhakikisha wanachukua hatua stahiki dhidi ya waliohusika na mauaji ya kinyama ya Alphonce Mawazo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita.

“Mawazo ameuawa kinyama, polisi wasipochukua hatua kwa watu waliofanya mauaji hayo tutachukua hatua wenyewe. Imeshaelezwa kwamba wahusika wanajulikana tena kwa majina. Sasa watu hawawezi kusubiri haki kama wanaona vyombo husika vya kutenda haki vinashindwa kufanya kazi yao,” alisema Lowassa.

Aliongeza kuwa sababu za kipindupindu zilizotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza hazikuwa na mashiko bali walilenga katika kutafuta namna ya kutumia magari yaliyonunuliwa wakati wa uchaguzi.

“Hata Biblia inasema waacheni watu wazike wafu wao. Uamuzi wa mahama Kuu utakuwa somo kwa nchi nzima. Mimi nampongeza Jaji aliyeruhusu watu kumuaga Mawazo,” alisema.

Naye Waziri Mkuu wa Zamani, Frederick Sumaye alieleza kusikitishwa na hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi kuzuia wafuasi wa Chadema kuaga mwili wa Mawazo katika jiji hilo. Alidai kuwa hali hiyo ilimuumiza zaidi kuona haki ya wananchi ikikandamizwa katika nchi huru, kitendo alichodai kilichangia kumfanya atoe machozi licha ya kuwa mgumu wa kutoa machozi hata alipofariki baba yake mzazi.

“Mimi ni mgumu sana wa kutoa machozi, hata baba yangu alipofariki sikutoa machozi. Lakini leo nimetoa machozi kwa sababu nchi ambayo ilikuwa na misingi ya amani, leo tunashuhudia watu wanadai haki wanauawa, ni jambo la kusikitisha,” alisema Sumaye.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alieleza kuwa wamepanga kufungua kesi ya madai dhidi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ili arudishe gharama za kuwaweka Mwanza mawaziri wakuu wa zamani wawili kwa muda wa siku nane wakisubiri kuuaga mwili wa Mawazo.

Wamiliki wa Maduka Ya Dawa Baridi Walia Na Kasi Ya Magufuli
Picha: Hii Ndio Zawadi Ya Uhuru Kenyatta Kwa Papa Francis Alipoingia Kenya