Baadhi ya wamiliki wa maduka makubwa ya madawa jijini Dar es Salaam wameanza kuona dalili za kuporomoka kwa biashara zao kufuatia kasi ya serikali ya awamu ya tano katika sekta ya afya, Dar24 inaripoti.

Taarifa ambazo Dar24 imezipata kutoka kwa wafanyakazi wa baadhi ya maduka hayo makubwa jijini humo, zimeeleza kuwa wamiliki wa maduka hayo wanatarajia kupungua kwa wateja wao kwa kiwango kikubwa endapo maelekezo ya Rais Magufuli yatafanyiwa kazi ipasavyo.

Rais Magufuli aliagiza kuwa Bohari ya Dawa (MSD) ifungue maduka makubwa katika hospitali zote kubwa nchini na ziwe na dawa zote muhimu kwa ajili ya wananchi kupata huduma hiyo badala ya kutegemea maduka binafsi.

“Hiyo ikitekelezwa nakwambia hatutapata kitu, ina maana hata wateja wetu waliokuwa wanakuja na bima za afya (NHIF) watakuwa wanaelekezwa kwenda kwenye maduka hayo ya serikali ambako dawa zitakuwa bei nafuu zaidi,” alisema mfanyakazi wa duka moja kubwa la dawa lililoko wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akitoa maagizo ya Rais Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa dawa zote muhimu zitapatikana kwenye maduka hayo ili wananchi waweze kupata dawa wanazohitaji.

“Labda mwananchi mwenyewe awe ameamua vinginevyo, labda katika duka la MSD kuna dawa kwa mfano kutoka nchini China lakini yeye anapenda kutumia ya nchi nyingine,” alisema Balozi Sefue.

Uamuzi huo wa serikali utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuwa watakuwa na uhakika wa kupata dawa elekezi.

Maneno Ya Mtoto Wa Marehemu Mawazo Yaliyowatoa Machozi Waombolezaji, Lowassa Ajitolea Kumsomesha
Lowassa Awatahadharisha Polisi Kifo Cha Mawazo, Mbowe Kufungua Kesi Nyingine