Joto la kinachoendelea visiwani Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa ZEC kutangaza kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, hususan baada ya tangazo hilo kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali hali iliyoashiria kuwa uchaguzi huo kweli umefutwa rasmi.

Kufuatia hali hiyo, aliyekuwa mgombea urais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad jana alifanya mkutano wa faragha jijini Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa pamoja na viongozi wengine wa Ukawa kuzungumzia kinachoendelea visiwani humo.

Baada ya kikao hicho cha faragha kilichofanyika katika ofisi ya Lowassa, Maalim Seif na Lowassa waliongea na vyombo vya habari lakini hawakuweka wazi uamuzi waliofikia baada ya kikao hicho. Waliwaeleza waandishi wa habari kuwa Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu ataeleza kila walichokubaliana kwenye kikao hicho kesho (Jumapili) atakapofanya mkutano na waandishi wa habari majira ya saa tano asubuhi.

Hata hivyo, Maalim Seif alieleza kuwa msimamo wa CUF uko palepale kuwa hawakubaliani na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi huo na kwamba hata Tangazo lililochapishwa kwenye gazeti la seriklai linaeleza wazi kuwa sio serikali iliyosema bali ni Mwenyekiti wa NEC, Jecha Salum Jecha.

Alisisitiza kuwa hawatashiriki tena uchaguzi wa Zanzibar kwani tayari ulikamilika na wanasubiri tu Tume iendelee na utaratibu wa kutangaza matokeo ambayo anaamini kuwa yeye ndiye mshindi kutokana na nyaraka za matokeo alizokusanya kwenye vituo vyote.

“Hata ukisoma tangazo la serikali linasema mimi Salum Jecha nimefuta uchaguzi, na si Serikali,” alisema Maalim Seif.

Kuhusu mazungumzo yake na Dkt. Ali Shein, Maalim Seif alisema kuwa ataeleza kuhusu hayo yote muda muafaka utakapofika.

Kwa upande wa Edward Lowassa, yeye aliingilia swali lililoulizwa na waandishi wa habari kutaka kufahamu mtazamo wa Maalim Seif kuhusu maoni ya baadhi ya watu kutaka itangazwe hali ya hatari Zanzibar, ambapo alisema suala hilo ni vyema wakamuuliza Rais John Magufuli kwa madai kuwa ndiye mwenye majibu sahihi. Naye Maalim Seif alisema kuwa anadhani bado hatujafika huko.

“Tumekuwa na mazungumzo na Maalim Seif mazuri sana nay a kushauriana kuhusu masuala ya Zanzibar na Jumapili tutatoa msimamo wetu,” alisema Lowassa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abadallah Safari, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima, Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwange.

Magufuli Kiboko, Afuta Kitengo Cha ‘Msosi’ Wa Rais Ikulu
Zlatan Atamba Kulipaisha Soka la Ufaransa