Rais John Magufuli ameendelea kufanya mabadiliko kwenye mfumo uliokuwepo ambapo sasa ameufumua muundo wa ofisi za Ikulu iliyoko Magogoni jijini Dar es Salaam.

Mmoja kati ya maafisa wa Ikulu waliliambia gazeti moja la kila siku kuwa Rais Magufuli alitembelea ofisi zilizoko Ikulu na kubaini kuwa zipo baadhi ya ofisi ambazo alidai hazina tija kwake hivyo aliamua kuzifuta.

Moja kati ya ofisi zilizofutwa ni kilichokuwa kitengo cha lishe ya Rais na kitengo maalum cha kupokea wageni binafsi wa Rais.

“Rais Magufuli alipoingia tu Ikulu alifanya ziara ya kukagua ofisi zote zilizopo Ikulu, alitaka kujua utendaji kazi wa ofisi hizo lakini alipofika kwenye kitengo maalum cha lishe ya Rais alisema haoni umuhimu wa kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu suala la lishe yake siku zote inasimamiwa na mkewe Janeth, akaamuru ifungwe na watumishi wake warejeshwe walikotoka,” anakaririwa Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mkuu wa kitengo cha Lishe kilichofutwa alirudishwa kwenye ofisi yake ya awali ambayo ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii huku maafisa wengine pia wakirudishwa katika wizara walizokuwa wakifanyia kazi awali.

Huu ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi zake za kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya wizara na baraza la mawaziri.

 

Watanzania Waishio Thailand Wachagua Viongozi Wao
Lowassa: Hili Muulizeni Magufuli