Mkuu wa benchi la ufundi la Young Africans, Luc Eymael amesema kama mambo yatakwenda kama anavyotarajia, kikosi chake kitakua na sura ya kutisha kuanzia msimu ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Eymael ametamba kwa kujiamini kwamba, akili yake kwa sasa ipo kwenye ushambuliaji na winga zote mbili katika usajili mpya.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji ameshamalizana na baadhi ya wachezaji na anashukuru kwamba, uongozi chini ya udhamini wa GSM wanakwenda kasi katika kuhakikisha mapendekezo ya wataalamu wa benchi la ufundi yanafanyiwa kazi.
Akizungumza moja kwa moja kutoka Ubelgiji alipo kwa sasa, Eymael amesema anataka timu yenye kasi na watu wa kazi ambayo hata straika aina ya Bernard Morrison awe anasota kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.
Pia, amesema hata mchezaji anapokosekana kikosi basi hakuna pengo kutokana na waliopo kuwa na uwezo wa kuziba nafasi hiyo na mashabiki wanafurahi.
Alisema anamhitaji pia kiraka Mbelgiji, Andrea Fileccia anayechezea klabu ya ridhaa ya daraja la kwanza nchini humo ya Royal Francs Borains.
“Nataka kuwa na wigo mpana hasa kule mbele, yaani aliyeko ndani na aliyeko benchi wote wawe na ubora stahiki wenye hadhi ya kuichezea Yanga.
“Huyu Andrea ni kama Morrison makali yake, lakini yeye ana uwezo wa kucheza hadi nafasi ya mshambuliaji wa kati. Huyu sehemu ni Morrison na sehemu ni Nchimbi,” alisema akimaanisha kwamba, anaweza kucheza pembeni na katikati, ana asisti na kufunga.
Eymael alisema akipata saini za washambuliaji na mawinga wa kigeni kutoka DR Congo, Ghana na Rwanda aliowapendekeza pamoja na wale wazawa, basi Young Africans itakuwa moto kweli kweli.
“Nikiwa na Morrison (Benard), Nchimbi (Ditram) na wengine wapya, ninataka kuwa na kikosi bora ambacho kitakuwa kinapata matokeo mazuri kila mechi,” alisisitiza Eymael.
Mpaka sasa Young Africans ina uhakika wa kuwapa mastaa wawili kutoka DR Congo kwenye ushambuliaji ambao ni Tuisila Kishinda wa AS Vita na Mpiana Mozizi wa FC Lupopo.
Kocha huyo amesisitiza msimu huu wakirejea uwanjani amepanga kuukamilisha kwa heshima ya aina yake kwa vile nafasi yao ya ubingwa ni finyu, lakini akili zao zipo kwenye kombe la FA.
Anasema kwamba lazima wabebe FA ili kupata aina ubora wa wachezaji anaotaka kwani wengi kigezo chao cha kusajiliwa ni shauku ya kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.