Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba zimesaini Hati za Makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya elimu ya juu kwa kubadilishana wakufunzi na wanafunzi, kufundisha lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana nchini Cuba pamoja na kutengeneza kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Stephen Byabato kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Dkt. Walter Garcia Jijini Havana na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Valdes Mesa.
Mbali na Makubaliano ya elimu, makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam na Chuo Kikuu cha Havana ambapo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kiliwasilishwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. William Anangisye wakati Chuo Kikuu Cha Havana kiliwasilishwa na Prof. Miriam Garcia
Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia wahadhiri, wanafunzi, tafiti, sayansi, teknolojia, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana na kutengeneza kamusi ya lugha ya Kiswahili na Kispaniola ili kusambaza matumizi ya lugha ya kiswahili nchini Cuba na nchi nyingine zinazozungumza lugha ya Kihispaniola.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amesema Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano hayo ambayo yanatoa mwongozo maalum wa jinsi ya kutekeleza mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.
Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknojia na Wizara ya Elimu ya Juu ya nchini Cuba ambayo yatawezesha ubadilishanaji wa wanafunzi, wahadhiri na watafiti katika eneo la sayansi na teknolojia ili kuwawezesha wahusika kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo hayo na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa pande zote mbili.