Waasi wa kundi la wapiganaji wa M23 wanadaiwa kuwauwa raia 131 katika eneo la mashariki mwa nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Novemba 29 na 30, 2022.
Madai hayo, yametolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo MONUSCO, kupitia matokeo ya uchunguzi wa awali, unaoonesha kuwa waliuwawa ikuwa ni sehemu ya mauaji ya kulipiza kisasi kwa raia.
MONUSCO imeongeza kuwa, waliouawa ni wanaume 102, wanawake 17 na watoto 12 na walipigwa risasi za moto au silaha zengine bila kujali athari za matokeo.
Aidha, Umoja wa Mataifa UN, umesema watu wanane walijeruhiwa kwa risasi na wengine 60 kutekwa nyara huku karibu wanawake 22 na wasichana watano wakibakwa.
Hata hivyo, Serikali jijini Kinshasa imesema watu 300 takriban wote wakiwa ni raia walifariki dunia katika mashambulizi ya M23 katika kijiji cha Kishishe kilichopo Mkoa wa Mashariki wa Kivu Kaskazini huku M23 ikikanusha kuhusika na mauaji hayo.