Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, imetoa hukumu ya kunyongwa kwa watu watatu Haruna Ndayanze mkazi wa kijiji cha Pozamoyo Wilayani Kaliua, Mtoni Kambogo na Ally Shaban na Ally wakazi wa kijiji cha Igalula Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, waliokuwa wanakabiliwa na kesi tofauti za mauaji.

Akisoma hukumu hiyo hii leo Desemba 8, 2022 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Tabora, Demetrio Nyakunga ambaye alikasimiwa mamlaka ya ziada ya kusikiliza mashauri ya mahakama kuu amesema katika shauri la kwanza Mahakama hiyo, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa Haruna Ndayanze baada ya kumtia hatiani kwa kumuua Kusaga Magulu.

Aidha, upande wa mashitaka uliokuwa ukiwakilishwa na mawakili Mwerito Ukongoji na Sabrina Silayo, uliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 25, 2020 katika kijiji cha Pozamoyo wilayani Kaliua ambapo siku hiyo alitimiza nia hiyo ovu kwa kumkata panga shingoni, mikononi na mwilini mtoto wa mkewe aliyezaa na mwanaume mwingine.

Mashahidi 12 wa upande wa mashtaka waliiambia Mahakama kuwa, sababu za mauaji hayo ni kutokana na mshitakiwa kumkuta mkewe, Stephania Alphonce, akimeza vidonge vya kufubaza virusi vya Ukimwi ambapo katika shauri la pili, Hakimu Nyakunga amewahukumu kunyongwa hadi kufa Ally Shaban Kinyogoli na Ally Mtoni Kambongo kwa kuwakuta na hatia ya kumuua Ally Rajabu.

Mahakama hiyo, iliambiwa na upande wa mashtaka kupitia kwa mashahidi wanane kuwa, washitakiwa walitenda kosa hilo Machi 22, 2020 huku katika shauri jingine, Mahakama kuu ikimuachilia huru, Zengo Kulwa mkazi wa kijiji cha Izugawima cha Wilayani Uyui, aliyekuwa akituhumiwa kwa kosa la kumua Joseph Elias, kutokana na kutojitosheleza kwa ushahidi.

Picha: Matukio mbalimbali Mkutano Mkuu wa CCM-Dodoma
Serikali kuendeleza usimamiaji ilani ya CCM