Timu ya maafisa waandamizi kutoka Marekani imewasili nchini Korea Kaskazini kwa lengo la kujadili kuhusu mkutano wa kihistoria kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong-un ambao wiki iliyopita ulikuwa na hatihati ya kufutwa.
Taarifa za kuwasili kwa timu hiyo ya Marekani nchini Korea Kaskazini zimetolewa jana na Rais Trump kupitia akaunti yake ya Twitter.
“Timu yetu ya maafisa wa Marekani imewasili nchini Korea Kaskazini kufanya maandalizi ya mkutano kati yangu na Kim Jong Un,” Trump
“Ninaamini kabisa kuwa Korea Kaskazini wanayo nafasi na watakuwa taifa lenye maendeleo makubwa kiuchumi siku moja. Kim Jong Un amekubaliana na mimi katika hilo. Itafanyika!,” ameongeza.
Pande zote, Idara ya Marekani pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini zimeeleza kuwa maafisa wake walikuwa kwenye majadiliano kuhusu mkutano wa Trump na Kim Jong-un.
Ingawa Trump alitangaza wiki iliyopita kuwa hakutakuwa na mkutano kati yake ya Kim Jong un hivi karibuni, maandalizi yanayofanywa yanaonesha mkutano huo uko palepale na huenda ni Juni 12 nchini Singapore kama ilivyokuwa imetajwa awali.
Timu ya maafisa kutoka Ikulu ya Marekani imesafiri kwenda nchini Singapore kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mkutano huo.